MKUTANO MKUU WA 10 WA KAUKI

MKUTANO MKUU WA 10 WA KAUKI
Tangazo la Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

KAUKI-Kidamali, Iringa

KAUKI-Kidamali, Iringa
Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

Friday, January 27, 2017

SHUKRANI KWA WANAUKOO - KANDA YA IRORE



Uongozi wa Umoja Wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), kwa niaba ya Wana Ukoo wote, unawashukuru wote waliofanikisha Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI, uliofanyika Vilalo, Kanda ya Irore, Mkoani Iringa, tarehe 2 Julai 2016. Tunatambua kuandaa mkutano wowote ni gharama, hivyo tunawapongeza kwa kujitoa kwao. Ni shughuli inayohitaji raslimali watu, fedha na zana ili kuweza kufikia lengo. Ni jambo la kujivunia na pia kutia moyo kwa wale wote ambao wameshiriki kikamilifu na kwa hali na mali katika jukumu hili. Licha ya kuwepo kwa watu wachache walioshiriki katika maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI, lakini umeweza kufanyika kwa mafanikio.



KAUKI pia inatoa shukrani za pekee kwa Uongozi wa KAUKI Kanda ya Irore, kwa kuhamasisha Wana Ukoo kushiriki kikamilifu katika maandalizi na pia kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI. Shukrani za pekee ziwaendee Ndugu Castory Kivenule, Pius Kivenule, Benard Kivenule, Amalia Kivenule, Michael Mateka na Wanaukoo kwa ujumla kwa moyo wao wa upendo na ukarimu, kwa kuamua kubeba jukumu hili. Uongozi wa KAUKI unawashukuru pia wanaukoo wote toka Kanda nyingine za Kidamali, Dar es Salaam na Kalenga kwa ushiriki wao. Pengine, kutokuwepo kwao, Mkutano huo usingeweza kufanikiwa.

Mwisho, shukrani za pekee ziwaendee ndugu zetu walioshiriki Mkutano Mkuu wa 11 kwa mara ya kwanza. Hii inaonesha dhamira yao ya dhati ya kuendelea kushirikiana na Wana Ukoo wenzao. Hali kadhalika wameonesha shauku ya kutaka kuujua ukoo na kuwafahamu wenzao.

Asante,

Imeandaliwa na:

Adam Kivenule
Katibu Mkuu, KAUKI

Thursday, December 17, 2015

MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU WA 11 WA UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)



Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI) kwa kushirikiana na Kanda ya Nduli, kwa heshima kubwa unapenda kuwajulisha ndugu, jamaa, marafiki na Wana Ukoo wote, umeanza maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI, utakaofanyika Kijijini Nduli, Mkoani Iringa, tarehe 2 had 3 Julai, 2016.

Kwa taarifa hii, tunaomba Viongozi wote wa KAUKI na Viongozi wa Kanda, kuanza kujiandaa kwa Mkutano huo muhimu. Sambamba na hilo, Viongozi wa KAUKI waendelee kuratibu maandalizi ya Mkutano kwa kusambaza taarifa na kuweka mikakati imara ya kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI unafanikiwa. Wadau wakuu wa maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI ni Viongozi wa Kanda kwa kushirikiana na ndugu wote.

Ikumbukwe kuwa, mwaka huu (2015), Mkutano wa Mkuu wa KAUKI uliopangwa ufanyika Kijijini Irore, Mkoano Iringa, umeshindwa kufanyika kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu. Maana nyingine Kanda ya Irore bado inayo nafasi nyingine ya kuandaa Mkutano Mkuu wa 12 wa KAUKI, 2017. Kwa hiyo wana Irore na sehemu zote za Igominyi mnaombwa kuanza kufanya maandalizi ya mkutano wenu, sambamba na maandalizi ya Mkutano Mkuu utakaofanyika Nduli mwakani.

Kuna mambo mengi muhimu yanaweza kufanyika kama sehemu muhimu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI, utakaofanyika Kijijini Nduli:
1. Kila ndugu kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI na kuhakikisha kuwa unafanikiwa. Kila mwana ukoo anaweza kujitoa kwa chochote kile ambacho kitasaidia kufanikisha Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI.
2. Ndugu wenye uwezo kujitolea ili kufanikisha Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI. Kuna wana Ukoo ambao wamejiajili na wana vipato vya uhakika. Tunaomba kwa moyo wa upendo wasaidie kuandaa mkutano huu. Pia kuna ndugu ambao wameajiliwa na wana vipato vizuri. Tunaomba wachukue jukumu la kusaidia kugharama za maandalizi ya Mkutano huo.
3. Wana Ukoo wa Kanda ya Nduli na Kanda nyingine ambazo zina fursa ya ardhi, wanaweza kulima angalau nusu ekari kwa lengo la kupanda mazao ambayo yatatumika kwa ajili ya kufanikisha Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI. Mazao ambayo yanaweza kupandwa ni pamoja na Mahindi, Maharage, Viazi na mazao mengine ya nafaka.
4. Kuhamasishana na kuhimizana ndugu na wana ukoo miongoni mwetu ili kuendelea kuwa na moyo wa kupendana, kushirikiana na kusaidiana; na pia kuwa pamoja katika masuala yote yanayohusu ndugu na ukoo kwa ujumla kwa faida yetu wote.
Matarajio ya Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI, utakaofanyika tarehe 2 – 3 Julai, 2016, Kijijini Nduli.
Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI unatarajia yafuatayo:
1. Kuendelea kuboresha Kitabu cha Wana Ukoo kwa kujaza taarifa mbalimbali za ndugu (Clan Organization Tree).
2. Kuwafahamisha wana ukoo, Historia na Chimbuko la Ukoo. Hususani Ukoo wa Kivenule.
3. Mwingiliano wa Ukoo wa Kivenule na Koo nyingine uliopelekea kuwepo kwa Ukoo wa Kivenule.
4. Kufanya tathmini ya mipango mbalimbali ya KAUKI tuliyojiwekea kwa miaka kadhaa.
5. Kutathmini changamoto na vikwazo mbalimbali vinavyoukabili Umoja wetu.
6. Yatakayojiri katika Mkutano Mkuu wa 11 wa KAUKI, utakaofanyika tarehe 2 – 3 Julai,

Imeandaliwa na kusambazwa na:

Katibu Mkuu (Adam Alphonce Kivenule)
Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI)
Mobile: 0713 270364
            kivenule@gmail.com



Monday, December 8, 2014


HOTUBA YA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA 10 WA KAUKI, JUNI 28 – 29, 2014, KIDAMALI – IRINGA

 

Ndugu Mgeni Rasmi, Ndugu Wageni Waalikwa; Wanaukoo na Jamii yote inayounda KAUKI;

Ndugu Majirani, Marafiki na Jamii yote Iliyojumuika Nasi; Mabibi na Mabwana;

 

Kamwene…, Munogage…, Makasi…,

 

Awali ya yote, nimwombe Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, uzima na Baraka, awape nguvu, afya na amani, wote mliokusanyika katika Mkutano huu wa 10 wa KAUKI. Pili, nimwombe Mwenyezi Mungu, awaepushe na hatari, rapsah na ubaya wowote ulioelekezwa kwenu; awalinde kutoka saa hii ya ufunguzi wa Mkutano hadi kesho wakati wa kuhitimisha shughuli hii muhimu kwa mwaka huu 2014.

 

Tatu, nawaomba wote tusimame kwa dakika moja (1) kuwakumbuka ndugu zetu ambao wametangulia mbele ya haki kutoka mwaka jana hadi mwezi Juni mwaka 2014. Ndugu waliotangulia mbele za haki ni:

1.   Agnes Mapembe, Mtoto wa Marehemu Sandra Kivenule, Mjukuu wa Kavilimembe Tavimyenda Kivenule

 

Mwenyezi Mungu azilaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.

 

Baada ya utangulizi huo mfupi, ni furaha kubwa kujumuika na hadhara hii siku ya leo.  Ni matumaini yangu kuwa wote ni wazima wa afya na pia uwepo wenu unaonesha namna mnavyothamini shughuli hii muhimu itakayofanyika kwa muda wa siku mbili; yaani leo na kesho, hali kadhalika kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI unafakiwa.   

 

Ni furaha iliyoje kuwa nanyi katika hadhara hii. Ni matumaini yangu kuwa, wote ni wazima wa afya na kuwepo kwenu pia kuonesha jinsi mnavyothamini shughuli ambayo tutaifanya kwa siku mbili, yaani leo na kesho katika kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu wa Kumi wa KAUKI unafanikiwa.

 

Ndugu Mgeni Rasmi;  nianze kutoa historia fupi ya umoja huu. KAUKI ni Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulioanzishwa rasmi mwaka 2005, kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo, zinazoikabili jamii inayounda umoja huu; hususani katika kujikwamua na ugumu wa maisha na pia kutumia fursa zinazopatikana ili kukabiliana na kuondokana na wimbi la umaskini, ujinga, maradhi na utegemezi. Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), ulianzishwa rasmi mnamo Desemba 17 - 18, 2005 Kijijini Kidamali. Harakati za kuanzishwa kwa KAUKI zilianza mwezi Februari 06, 2005 Jijini Dar es Salaam kwa kufanya mkutano wa kwanza wa mashauriano. Harakati nyingine na kuunda kamati za maandalizi zilielekezwa upande wa Kidamali, Ilole na Nduli. Kwa upande wa Kidamali, Mkutano wa kwanza wa maandalizi ya Mkutano Mkuu ulifanyika mwezi Mei ambapo wajumbe toka Dar es Salaam walishiriki katika majadiliano, kuchagua viongozi wa kuunda kamati ya maandalizi na kuhamasisha.

 

Ndugu Mgeni Rasmi; Umoja wa Ukoo wa Kivenule ulizinduliwa rasmi mwaka 2006, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo wa Kivenule uliofanyika tarehe 24 – 25 Juni 2006 katika Ukumbi wa Sanga Kijijini Kidamali, Iringa. Kuzinduliwa kwa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, kulienda sambamba na uzinduzi wa Mfuko wa Ukoo pamoja na Kuipitisha Rasimu ya Katiba ya Umoja wa Ukoo wa Kivenule na kuwa Katiba Rasmi; hivyo kutoa fursa ya kuanza kwa utekelezaji wa shughuli na mipango mbalimbali ya maendeleo. Pia, pamoja na mambo mengine, katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Ukoo, kulifanyika uchaguzi wa Viongozi wa Kanda, uchaguzi wa Walezi wa Ukoo na hivyo utendaji rasmi wa KAUKI kuruhusiwa kuanza.

 

Ndugu Mgeni Rasmi; Huu ni Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI; na tayari mikutano mingine Nane imekwisha fanyika, mitatu kijijini Kidamali na mkutano moja kijijini Irole, Nduli, Igowole-Mufindi na Jijini Dar es Salaam na Mikutano 2 Magubike,. Huu ni mzunguko mwingine tena baada ya kumaliza kanda zote. Pengine mkutano huu utashauri namna nyingine ya uendeshaji wa mikutano ya namna hii.

 

 

 

Malengo ya KAUKI

Ndugu Mgeni Rasmi; malengo makuu ya KAUKI ni kujaribu kwa kila hali kwa kutumia ujuzi na maarifa, kuinua uwezo wa kielimu, kiuchumi na kimaendeleo, kwa wanajamii wanaounda umoja huo, kwa kutumia rasilimali mbalimbali zinazopatika katika nchi ya Tanzania na hususani katika maeneo wanayoishi; ikiwa ni pamoja kuihamasisha jamii hii kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kupunguza umaskini unaowakabili.

 

KAUKI imeanzishwa kukidhi shida na mahitaji ya jamii iliyounda umoja huu na hususani katika maeneo lengwa ya elimu, afya, uchumi na maendeleo, kwa kushirikisha mawazo, fikra, ujuzi na maarifa ya kila mwanaukoo, katika mikutano mikuu na mikutano midogo midogo, ambayo inaandaliwa na wanaukoo wenyewe. Kwa kukutana pamoja, fikra za kujenga, ujuzi, uzoefu, kujengewa uwezo na maarifa, huunganishwa pamoja na kisha kupanga mikakati mbadala ya kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha.

 

Ndugu Mgeni Rasmi; malengo KAUKI ni mengi na baadhi yake ni:

·        kuwa na ofisi yake Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda

·        Kuisajili KAUKI na kuwa na mfuko wa kusaidia ndugu katika elimu, afya na matatizo mengine. Tayari mfuko umeanzishwa na unaendelea kuchangiwa. 

·        kuwa na sanduku lake la posta, tovuti. Kwa sasa ina tovuti  inayopatika kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com na inaboreshwa kupitia www.tagumtwa.blogoak.com  na www.kauki-kauki.blogspot.com   

·        Kuwa na Akaunti katika Benki – tayari imefungua katika Benki ya NMB, Iringa Mjini

·        kuwa na vitendea kazi mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti

·        kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa wadau wake. Inatoa elimu katika mikutano yake

·        kubuni na kutekeleza miradi ambayo itawasadia wanajamii. Mpango wa Mradi wa Alizeti-Irole, ambao bado haujaanza kutekelezwa.

·        kuwa na kitengo cha Utaalam wa Kitaaluma na Kiujuzi ambacho kitafanya shughuli za kuiletea fedha KAUKI, pamoja na miradi mbalimbali. Ipo katika mchakato.

·        Kuchapisha kitabu toleo la kwanza cha Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa kipindi cha mwaka 2009-2013. Kazi inaendelea na taarifa mbalimbali zinaendelea kukusanywa.

 

Mafanikio

Ndugu Mgeni Rasmi; KAUKI imefanikiwa kufanya yafuatayo:

·        kuendelea kufanyika kwa mikutano mkuu. Mikutano Mikuu Tisa tayari imefanyika Kidamali mara tatu, Magubike mara tatu, Irole, Nduli, Igowole-Mufindi na mara moja moja.

·        kupanua wigo wa ushiriki kutoka Irole, Nduli, Itagutwa, Mgongo na Mufindi; Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro na maeneo mengine.

·        Kuongezeka kwa ufahamu na uelewa wa watu kuhusu KAUKI na mada zinazofundishwa

·        Kufahamiana baina ya wana-KAUKI kumeongezeka mara dufu

·        Kuanzishwa kwa Mfuko wa KAUKI

·        Imeanzisha blogs ambazo zinabeba taarifa mbalimbali za KAUKI na wana-KAUKI kwa ujumla.

 

Changamoto

Ndugu Mgeni Rasmi; Changamoto zinazoikabili KAUKI ni pamoja na

·        Ushiriki duni wa wanaukoo katika mikutano mikuu.

·        Kasi ndogo na moyo wa kuchangia mfuko wa kusaidia wanaukoo

·        Kutokidhi gharama za kuandaa mikutano hii kwa sababu michango inakuwa ni kidogo

·        Kutofikia malengo ya mipango tunayojiwekea

·        Ndugu wa mijini kuwa na mwamko mdogo wa kuunga mkono jitihada hizi

 

 

Matarajio katika Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

Ndugu Mgeni Rasmi; Kama Ratiba inavyoonesha, hayo ndiyo yatakayofanyika katika siku mbili za Mkutano Mkuu wa Kumi wa KAUKI. Lakini, tunategemea kuwa na Mada kadhaa ikiwemo ya Chimbuko Historia ya Ukoo ambapo tutaijadili kwa undani zaidi. Lakini pia, masuala mengine mfano elimu, maendeleo na ushirikiano wa dhati baina ya wanandugu yatapewa kipaumbele.

 

Utambulisho baina ya wanaukoo utafanyika kwa kina na kila ndugu/mwanaukoo atakuwa na kitambulisho ambacho atakivaa kifuani kwake. Kutakuwa na fursa mbalimbali kwa wanandugu kupeana uzoefu mbalimbali wa utafutaji wa maisha bora. Mbinu za kujiinua kimaisha zitafundishwa na wadau wenye uzoefu pamoja na aina mbalimbali za miradi ambayo ndugu wanaweza kufanya.

 

Tutakuwa na kipindi cha kupeana uzoefu wa shughuli mbalimbali za kiuchumi kutoka katika maeneo mbalimbali ambako ndugu wanaishi. Kama ilivyofanyika katika Mkutano Mkuu wa Tatu, Nne, Tano, Sita, Saba, Nane na Tisa wa KAUKI, maeneo yatakayotolewa uzoefu Kilimo, biashara na ajira kutoka katika maeneo mbalimbali. Kwa kupeana elimu ya ujasiliamali itasaidia kutufungua macho na hivyo kuongeza uwezo wa kufikiri na kwenda kutafuta maisha katika maeneo ambayo ni mbadala kwetu. Pia taarifa hizi zitawasaidia wanandugu toka maeneo mengine kupata mwanga wa shughuli mbadala zitakazosaidia kupata kipato na kuboresha maisha.

 

Matarajio ya Mbeleni

Ndugu Mgeni Rasmi; Mipango ya KAUKI kwa mwaka uliopita 2014 na 2015

·        Kuendeleza jitihada za kufungua ofisi Kidamali na kununua vifaa vya ndani ya ofisi kama vile kompyuta, printa na fenicha.

·        Kutafuta hati ya Kimila ya Eneo la Kihistoria la Mlafu

·        KAUKI kufuatilia kwa karibu suala la Elimu kwa Watoto katika Kanda

·        Kuchapisha kitabu cha historia ya wahehe ambapo ndani yake pia kutakuwa na taarifa za KAUKI.

·        Kuongeza wigo wa ushiriki katika mikutano; Kuhamasisha wana-KAUKI kuchangia mfuko

 

Hitimisho

Ndugu Mgeni Rasmi; KAUKI imeendelea kujikita katika kuongeza uangavu na weledi kwa wanaukoo kutokana na kutambua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika dunia hii ya ushindani. Ugumu wa maisha, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, na changamoto mbalimbali ambazo kila mwana-KAUKI anaiona, ameguswa nayo au kuathiriwa nayo. Tatizo la ufisadi wa raslimali za watanzania, rushwa katika huduma za jamii mfano kukosa dawa hospitalini, maji safi na salama, elimu duni na ukosefu wa ajira, vyote vinatuathiri sisi. KAUKI inaamini kuwa mwana-KAUKI mwenyewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ya kuamua hatma na mustakabali wa maisha yake ya sasa na baadaye. KAUKI haitarajii maisha bora kwa kila mwana-KAUKI au mtanzania mwingine yataletwa na wanasiasa au watu baki waliopo nje ya nchi yetu. Jukumu la maendeleo ni letu sisi wenyewe. Ndio maana tunahimiza watu kujitoa kwa hali na mali kuuchangia mfuko wetu ili uweze kuisaidia jamii yetu katika nyanja zote za kiuchumi, elimu, afya na maendeleo.

 

Ndugu Mgeni Rasmi, baada ya kusema hayo machache, kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu ya Kidamali, Iringa, inakuomba Ufungue Rasmi Mkutano Mkuu wa 10 wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI).

 

Karibu Sana

 

Imetolewa na:

 

Ndugu Faustino Kivenule

Mwenyekiti wa KAUKI

Kwa Niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu  wa 10 wa KAUKI